Hakuna bingwa wakati ligi ya Uholanzi ikiwa ya kwanza Ulaya kuufuta msimu

Shirikisho la kandanda nchini Uholanzi – KNVB limeufuta rasmi msimu wa 2019-2020, na kuifanya ligi kuu ya kandanda nchini humo kuwa ligi ya kwanza kuu barani Ulaya kufutwa kutokana na janga la virusi vya corona. Hakuna timu itakayotawazwa mshindi baada ya Ajax na AZ Alkmaar kubakia kileleni na pointi sawa huku ikiwa imesalia mechi tisa msimu kukamilika. Taariifa ya KNVB imesema kutokana na hatua zilizochukuliwa na serikali kuzuia mikusanyiko mikubwa, imekuwa vigumu kuumaliza msimu huu wa kandanda.

Imesema afya ya umma ni suala la kipaumbele.Vinara Ajax, ambao wako juu ya AZ kwa tofauti ya mabao, watafuzu katika ligi ya Mabingwa Ulaya, kwa mujibu wa KNVB lakini watasubiri uamuzi wa shirikisho la UEFA mnamo Mei 25. Hakuna timu itakayoshuka daraja wala kupandishwa daraja, na msimu ujao utaanza na timu 18 zilizokuwa katika ligi kuu msimu huu.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends