Hatima ya Ubingwa Simba, Upo Mikononi Mwa Yanga.

428

Japo ni mapema kwa sasa kuzungumzia ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara lakini nataka kuliweka hili wazi mapema kuwa ‘Hatima ya ubingwa Simba, upo mikononi mwa Yanga’ kivipi?

Tupo kwenye mzunguko wa 13 Tangia kuanza kwa msimu wa 2021/2022 na Yanga SC ndio yupo kileleni akiongoza kwa alama 35 huku mtani wake bingwa mtetezi Wekundu wa Msimbazi Simba akiwa nyuma kwa alama 10 na akiba ya mchezo mmoja(Kagera Sugar).

Kutokana na mwendelezo mzuri waliokuanao watoto wa Jangwani mabingwa wa kihistoria na muunganiko ambao Yanga wanao ni wazi kabisa ubingwa kwa Simba ambao wametwaa ubingwa kwa misimu minne iliyopita upo mikononi mwa Yanga.

Kwenye michezo ambayo mpaka hivi sasa Yanga imecheza haijapoteza mchezo hata mmoja huku ikiondoka na sare ya michezo dhidi ya Namungo na mpinzani wake Simba. Hapa kuna kitu nataka nikukumbushe ambacho ili uwe bingwa wa Ligi Kuu unatakiwa kukifanya.

Katika msimu uliopita, bingwa mtetezi yaani Simba alipoteza michezo mitatu na kutoa sare 5 na kumfanya awe bingwa kwa jumla ya alama 83 akiwa mbele kwa alama 9 dhidi ya mpinzani wake Yanga SC ambaye alimaliza kwa alama 74 akiwa na jumla ya sare 11 na kupoteza michezo 2

Kumbuka, wakati Simba anachukua ubingwa wake wa mara ya nne Simba ilikua ya moto kweli kweli huku Yanga wakionekana wakijitafuta tafuta kifedha hata ki mchezaji mmoja mmoja. Yanga sasa hivi inaonekana kuwa vizuri ki timu na ki ubora mchezaji mmoja mmoja, hapa kazi ipo.

Mpaka sasa ili Simba iwe kwenye nafasi mzuri itaombea zaidi mpinzani wake apoteze angalau michezo mitatu huku yeye akishinda kila mchezo wake ambapo ni ngumu kwa sasa Yanga kupoteza michezo zaidi ya mitatu, hasa ikichagizwa kuwa mechi ambazo alipoteza au kudondosha pointi msimu uliopita, msimu huu amevuna alama, mechi dhidi ya Coastal Union na Polisi Tanzania.

Miongoni mwa msimu mgumu kwenye Ligi kuu Tanzania Bara ulikua ni msimu wa mwaka ‪2016-2017‬ ambapo bingwa Yanga SC alimaliza kwa alama 68 akipoteza michezo 4 na kutoa sare michezo 5 huku mpinzani wake mnyama Simba SC akiwa amemaliza kwa alama hizo hizo 68 akiukosa ubingwa kwa magoli ya kufunga na kufungwa

Kwa takwimu hizo inakuonesha dhahiri kama timu mbili za juu zinazowania ubingwa ni angalau upoteze michezo miwili au mitatu na kutoa sare mbili au tatu ambapo tayari mnyama Simba kashapoteza kwenye mzunguko wa kwanza.

Sasa je kama tayari kashapoteza michezo yake hiyo na bado haongozi ligi basi ni wazi ubingwa kwa Simba upo mikononi mwa Yanga kwamaana Yanga ikipoteza mechi zaidi ya tatu basi Simba itaweza kutetea ubingwa wake kitu ambacho ni kigumu.

Author: Asifiwe Mbembela