Hazard aiambia kwaheri Chelsea kwa kuwapa zawadi

59

Ni mechi ambayo alitarajiwa kuitumia katika kuwaaga mashabiki wake. Na baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa, ndivyo mambo yalivyokuwa katika uwanja wa Olimpiki mjini Baku, Azerbaijan. Eden Hazard alifunga magoli mawili huku Chelsea ikiibamiza Arsenal katika fainali ya kombe la Ligi ya Europa na kumpatia kocha Maurizio Sarri kombe lake la kwanza tangu achukue usukani wa timu hiyo.

Olivier Giroud aliifungia Chelsea goli la kwanza dhidi ya klabu yake ya zamani kupitia kichwa safi huku Pedro akifunga goli la pili kupitia krosi ya Hazard.

Baada ya kutoa pasi ya bao la pili, raia huyo wa Ubelgiji alifunga penalti na kufanya mambo kuwa 3-0. Alex Iwobi aliipatia Arsenal bao la kufutia machozi mda mchache baada ya kuingia kama mchezaji wa akiba lakini Hazard alifunga krosi nzuri ya Giroud na kufanya mambo kuwa 4-1.

Huku uwanja ukiwa na mashabiki 5,000 kutoka pande zote mbili hali haikuwa shwari katika uwanja huo ulioonekana kujaa nusu nchini Azerbaijan.

Gunners watarudi katika Ligi ya Europa msimu ujao, lakini watacheza bila kipa Cech ambaye anatarajiwa kustaafu akiwa na umri wa miaka 37.

Hazard amedokeza kuwa amemaliza safari yake na klabu ya Chelsea. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ubelgiji amekuwa akihusishwa na tetesi za kuhamia Real Madrid na amesema kwa sasa “anasubiria klabu hizo (kukubaliana).”

“Nafikiri hii ni kwaheri ktoka kwangu, lakini kwenye mpira hauwezi kujua kitakachotokea.” Kocha wa Chelsea Maurizio Sarri amesema anaheshimu maamuzi ya Hazard.

Author: Bruce Amani