Henderson, Sterling kuikosa Iceland kutokana na majeruhi

Nahodha wa England Jordan Henderson na winga wa Manchester City Raheem Sterling watakosa mechi ya Ligi ya Mataifa Ulaya dhidi ya Iceland kutokana na wote kuwa majeruhi. England kesho Jumatano itashuka uwanjani kumenyana na Iceland ambapo imefahamika kuwa miongoni mwa nyota ambao watakosa mtanange huo ni Henderson na Sterling.

Nahodha wa Liverpool Henderson nafasi yake ilichukuliwa baada ya mapumziko katika kipigo cha goli 2-0 dhidi ya Ubeligiji, wakati Sterling alikosa mechi hiyo kabisa. Wachezaji hao wote watarudi katika vilabu vyao kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa majeraha yao ikiwa Ligi Kuu England inarejea wikiendi hii.

Manchester City watasafiri mpaka nyumbani kwa Tottenham Jumamosi na Liverpool iwapokea Leicester City Jumapili. Hata mchezo wa kesho utakuwa wa kukamilisha ratiba tu kwa England ambayo tayari imepoteza sifa ya kushiriki fainali za Ligi ya Mataifa mwezi Octoba mwakani kutokana na kipigo ilichokutana nacho dhidi ya Ubeligiji.

Author: Asifiwe Mbembela