Henry asherehekea ushindi wa kwanza na Monaco

Thierry Henry hatimaye ameonja furaha ya ushindi kwa mara ya kwanza kama kocha wa Monaco. Na atamshukuru Radamel Falcao aliyefunga bao la pekee na la ushindi kupitia mkwaji wa freekick ambalo liliwaangamiza Caen.

Mabingwa hao wa 2017 hawakuwa wameshinda mechi yoyote tangu Agosti 11 na walikuwa wametoka sare mechi mbili na kupoteza nne tangu Henry alipochukua usukani wiki sita zilizopita.

Ingawa ushindi huo haukuiondoa klabu hiyo katika eneo la kushushwa ngazi, angalau ilimuondolea Henry shinikizo kiasi. Monaco inabaki katika nafasi ya 19.

Wakati huo huo, Paris St-Germain iliifunga Toulouse 1-0 na kurefusha rekodi yao ya kutoshindwa mchuano wowote katika ligi tangu mwanzo wa msimu. Mabngwa hao wameshinda mechi zote 14 za ligi. Bao hilo la PSG lilifungwa na Edinson Cavani.

Author: Bruce Amani