Hersi Said awaita mashabiki Yanga

Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, injinia Hersi Said amewaomba mashabiki wa klabu ya Yanga kujitokeza kwa wingi kushuhudia na kutoa hamasa kwenye mtanange wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo Fc mchezo unaokusudiwa kupigwa Jumamosi saa 10 jioni.

Injini Hersi ameyasema hayo Leo Ijumaa baada ya kufanya mazungumzo ya takribani dakika 15 na wachezaji wa timu hiyo baada ya mazoezi ya kawaida, mazungumzo yaliyofanyika ndani ya uwanja huku mashabiki na Waandishi wa Habari wakizuiwa kusogea kwenye eneo hilo.

Injini Hersi Said amesema kama ni maandalizi ya nje ya uwanja tayari yamekamilika sawa na maandalizi ya ndani ya uwanja ambayo siku zote huangukia kwa kocha.

Hersi hakutaka kuweka wazi alichowaambia wachezaji katika kikao hicho lakini akawataka mashabiki kufika kwa wingi kesho kuishangilia timu yao kwani anaamini watapata ushindi.

“Mechi ya Namungo itakuwa ngumu kwani wamefanya usajili mzuri na pia wana uongozi mzuri lakini hata sisi tumejipanga kwani tuna kikosi bora na tunataka tuendeleza ushindi ili tuzidi kukaa kileleni kwenye msimamo wa Ligi” amesema Hersi ambaye ameingia hofu na hali ya Uwanja kuwa hauna ubora

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends