Hispania, Ureno waomba uenyeji wa Kombe la Dunia 2030

230

Mataifa ya Hispania na Ureno kwa pamoja yameomba kuwa wenyeji wa Kombe la Dunia mwaka 2030.
Alama ya kuomba ilifanywa na wachezaji wa timu hizo mbili kabla ya mchezo wa kirafiki uliopigwa Ijumaa na kumalizika kwa sare tasa katika dimba la Wanda Metropolitano nchini Hispania.
Mfalme Filipe wa Hispania na Rais wa Ureno Marcelo Rebelo De Sousa walikuwepo dimbani hapo na kusaini makubaliano ya kuomba kuandaa mashindano hayo makubwa kwa pamoja.
“Serikali ya nchi hizi mbili (Hispania na Ureno) inapenda kuonyesha matamanio yake ya kuwa wenyeji wa Kombe la Dunia 2030”, makubaliano hayo yalisema.
Kombe la Dunia la mwaka 2022 litafanyika Qatar, wakati Canada, Mexico na Marekani zitaandaa Kombe la Dunia 2026 kwa pamoja.
Shirikisho la Kandanda duniani Fifa limepanga kutangaza taifa mwenyeji wa Kombe la Dunia 2030 mwaka 2024.
Ushindani mkubwa kwa mataifa haya mawili unatoka kwa Uingereza, Ireland, Argentina, Uruguay, Paraguay na Chile ambao pia wamepanga kuomba kuandaa fainali katika mwaka husika.

Author: Bruce Amani