Imeshatokea, Paris Saint Germain wametawazwa kuwa bingwa wa Ligue 1 kutokana na virusi vya Corona kuendelea kuathiri shughuli za siku na siku ulimwenguni
Maamuzi hayo hayakuwa rahisi kufikiwa kwani kulikuwa na njia moja, mbili mpaka tatu ambazo zilitakiwa kupitiwa ili kutangaza rasmi uhalali wa PSG kama bingwa mpya wa taji hilo.
Mamlaka ya mpira zimeangalia mechi ambazo zimechezwa kuwa ni nyingi kuliko zilizobaki hivyo ubingwa utakuwa halali kwa timu kinara, pia wameangalia katika michezo hiyo 27 nani ambaye amevuna alama nyingi kati ya timu moja na nyingine (points per game).
Tayari maamuzi yameshachukuliwa lakini timu iliyoathirika zaidi na uhamuzi huo ni Lyon ambayo ilikuwa haijacheza mchezo mmoja huku nafasi pekee waliyonayo ni kushiriki mashindano ya Europa ligi msimu ujao baada ya michezo 27, hivyo walikuwa nafasi ya kwanza.
Nafasi pekee kwa Lyon kushiriki mashindano ya ligi ya mabingwa Ulaya ni kushinda kombe la ligi ambayo inaweza kuendelea hapo baadae kama kutatengamaa pia inaweza kufutwa, nafasi ya pili ni kushinda Uefa jambo ambalo sio rahisi kwa timu hiyo.
Wakati huo huo, PSG wamepewa taji hilo kiurahisi kwa sababu ya walikuwa mbele kwa alama 12 dhidi ya timu inayofuata, hii ni tofauti kidogo na Uholanzi ambako ligi haijatoa bingwa kutokana na kutokuwepo kwa utofauti wa alama kwa vinara wa ligi hiyo kwa maana ya Ajax na AZ Alkmaar.
PSG wana sababu moja ya kusherehekea taji hilo, lakini furaha ya mashabiki wa timu hiyo sio taji pekee la Ligue 1 bali kutwaa taji la Uefa ambalo limekuwa tamanio kwa mabosi na mashabiki wa timu hiyo.
Mpaka sasa haijulikani kama Uefa itachezwa lakini PSG wamesema wako tayari kucheza hata nje ya Ufaransa kwani miongoni mwa makusudi yao ni kushinda taji hilo msimu huu.
Jambo lingine gumu ambalo vilabu vyote Ufaransa vitakumbana navyo ni kukubali hasara ya mapato ya TV ambayo inatokana na kufupishwa kwa msimu.
