Homa ya Kariakoo derby yapanda, mashabiki wajitamba

Homa ya pambano la ligi kuu ya Tanzania la watani wa jadi kati ya Yanga na Simba imeanza kushika kasi kuanzia mashabiki, wachezaji na viongozi wa timu hizo ambapo mchezo huo utafanyika Jumamosi hii ya Feb 16 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 11 jioni.

Kuelekea mchezo huo shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetangaza viingilio vikiwa vimegawanywa katika makundi matatu ambapo kiingilio cha chini zaidi kitakuwa ni shilingi 7,000 kwa viti vya mzunguko.  Viingilio vingine katika mchezo huo vitakuwa ni shilingi 30,000 kwa VIP A na 20,000 kwa VIP B na C. Makocha wote wawili kwa nyakati tofauti walikanusha kuweka nguvu kubwa kwa mchezo ambapo kila mmoja anaonekana anajiandaa kikawaida.

Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera alikaririwa akizungumza na Waandishi wa Habari za michezo baada ya mechi dhidi ya JKT Tanzania akisema hajui kama mechi ijayo atacheza na Simba, “maandalizi nitakayofanya ni ya kawaida kama michezo mingine” alisema Mkongomani Zahera. Hali kadhalika, Patrick Aussems “Uchebe” akizungumza na Vyombo vya Habari kuelekea mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Ahly hapo kesho Jumanne  amesisitiza kuweka mawazo yake katika mchezo wa Ligi ya mabingwa zaidi.

Itakuwa mechi ngumu kutokana na matokeo ya hivi karibuni kwa timu hizo kwenye mashindano ya ndani ambapo Yanga inaongoza ligi kwa alama 59 na imetoka kushindi dhidi ya JKT Tanzania wakati Simba ipo nafasi ya tatu na imetoka kushinda dhidi ya Mwadui Fc zikiwa na tofauti ya mechi 7.

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends