Homa ya pambano la Man City Vs PSG usipime! Mbappe aongoza hofu

Kocha wa Manchester City Pep Guardiola amesema mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya matajiri Paris St-Germain ni mchezo wa kawaida kama ilivyo michezo mengine ambayo amekuwa akiicheza kwenye Ligi na mashindano mengine.

Kocha Guardiola anayasema hayo wakati ambao kikosi chake kitacheza dhidi ya PSG mchezo wa mkondo wa pili wa nusu fainali kufuatia ule kwanza kumalizika kwa faida ya Manchester City walioshinda bao 2-1.

Pep amesema mashindano ya Ligi ya Mabingwa yanahitaji umakini zaidi katika kutumia nafasi na kukubali kuteseka baadhi ya nyakati kutokana na upinzani uliopo.

Kwa upande wake kocha wa Paris St-Germain Mauricio Pochettino amesema bado hana uhakika kama mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa Kylian Mbappe mwenye umri wa miaka 22 atakuwa tayari kucheza mechi ya kesho baada ya kupata majeruhi kidogo.

Mbappe alikosa mechi ya Jumamosi dhidi ya Lens ambayo walishinda.

Mbappe amefunga jumla ya goli 37 katika mechi 43 ukijumulisha na bao 10 za Ligi ya Mabingwa Ulaya.

PSG wanahitaji kupindua meza kibabe kwa kutinga fainali baada ya msimu uliopita kufungwa na Bayern Munich hatua ya fainali kwa bao 1-0.

Hata hivyo, kupindua meza kunahitaji wachezaji kupunguza makosa binafsi na kuongeza ufanisi na matendo kwenye maeneo yote matatu muhimu uwanjani kama ulinzi, kiungo na ushambuliaji.

Author: Bruce Amani

Sharing is caring!

0Shares