Huyu Kinda Haaland ana balaa, aisaidia Dortmund kuipiga Cologne 5-1

Erling Braut Haaland ameendelea kuwa gumzo mbele ya vijiwe vya mashabiki, meza za wataalamu wa takwimu baada ya jana Ijumaa kufunga tena goli mbili katika ushindi wa Borussia Dortmund wa goli 5-1 dhidi ya Cologne mtanange wa Bundesliga.

Kinda huyo raia wa Norway amekuwa gumzo kwa sababu takwimu zake na umri wake waweza sema haviendani, amefunga goli 33 kwenye michezo 24 aliyocheza kwa ujumla msimu huu.

Akiwa amesajiliwa dirisha dogo la mwezi Januari na Dortmund tayari ameshafunga goli 5 kwenye mechi 2, ni sawa na goli moja kila baada ya dakika 12, cha ajabu goli zote amezifunga akitokea bechi yaani mchezaji wa akiba.

Anakuwa mchezaji wa kwanza ndani ya Bundesliga kufunga goli tano kwenye mechi mbili za mwanzo za ligi hiyo.

Haaland, 19, alifunga goli 28 kwenye mechi 22 akiwa na Red Bull Salzburg ukijumuisha na goli nane kwenye mechi sita za Ligi ya Mabingwa Ulaya, kabla ya Dortmund kuvunja kibubu cha paundi milioni 17 na kumchukua kinda huyo mwenye ajabu na takwimu.

Matokeo hayo yanaifanya Borussia Dortmund kufikisha alama 36 nafasi ya tatu sawa na Bayern Munich ambao nao wana alama 36 licha ya kwamba Bayern wanamchezo mmoja mkoni, pia wanafaida ya goli za kufunga na kufungwa. Kinara wa Bundesliga ni RB Leipzig wenye pointi 40.

Author: Bruce Amani