Infantino apinga La Liga kuchezwa Marekani

Rais wa Shirikisho la Kandanda Duniani – FIFA Gianni Infantino ameelezea mashaka kuhusu mpango wa Ligi Kuu ya kandanda Uhispania – La Liga kuandaa mchuano kati ya Girona na Barcelona nchini Marekani. Infantino amesema katika taarifa iliyotolewa na FIFA kwa televisheni ya ESPN kuwa anaona ni bora kutazama mchuano wa kuvutia na kusisimua wa ligi ya kandanda ya Marekani – MLS nchini Marekani badala ya mchuano wa La Liga kuchezwa Marekani. Anasema katika kandanda, kanuni ya msingi ni kucheza katika uwanja wa nyumbani mchuano wa nyumbani, na sio katika nchi ya kigeni.

La Liga inataka mchuano huo uchezwe mjini Miami Januari 26, 2019, lakini rais wa FIFA haungi mkono wazo hilo.

Ligi ya Uhispania imelitaka shirikisho la kandanda la Uhispania kuidhinisha mtanange huo kuchezwa ngambo, wakati vyama vya kandanda vya Marekani, UEFA na CONCACAF, ambacho kinawakilisha eneo la Amerika Kaskazini na Kati na Caribbean, lazima pia viridhie ili mipango hiyo iendelee.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends