Inter Milan wapunguzwa kasi na Sampdoria, wafungwa 2-1

273

Klabu ya Inter Milan imegota kigingi katika mbio za kumkamata kinara wa Ligi Kuu nchini Italia AC Milan baada ya kukutana na kichapo kutoka kwa Sampdoria katika mchezo wa Serie A uliopigwa leo Jumatano.

Inter walikuwa kwenye nafasi ya kuongoza walipopata pigo huru la penati lakini winga wa zamani wa Manchester United, Arsenal na Barcelona Alexis Sanchez alikosa penati yake iliyookolewa na mlinda mlango kabla ya mambo kuwa magumu upande wao.

Kipigo hicho kimehitimisha mfuatano wa ushindi kwa Inter ambao walikuwa wanahitaji ushindi kufikia mechi nane za Serie A wakiwa wamebakia na pointi zao 36 alama moja nyuma ya AC Milan ambao watakuwa na kibarua kizito mbele ya Juventus leo usiku.

Antonio Candreva, ambaye yuko kwa mkopo akitokea Inter na Keita Balde walikwamisha mpira nyavuni katika nyakati tofauti kuipa ushindi Sampdoria.

Stefan de Vrij alipunguza maumivu kwa inter Milan baada ya kufunga goli la kufutia machozi katika mchezo huo.

KWINGINEKO, ndani ya Serie A, Roma wamepata ushindi mnono wa goli 3-1 dhidi ya Crotone ambao walifungwa sita na Inter wiki iliyopita.

Borja Mayoral alifunga goli mbili na kiungo mshambuliaji wa zamani wa Manchester United na Arsenal Henrikh Mkhitaryan akafunga goli moja.

Author: Bruce Amani