Janga la Virusi vya corona lavuruga viwanja vya michezo

Michezo miwili ya Ligi Europa imepigwa chini kutokana na hofu ya Virusi vya Corona ambapo michezo hiyo ni pamoja na ule wa Sevilla na Roma uliotakiwa upigwe kesho Alhamis Hispania na ule wa Italia kati ya Inter Milan na Getafe.

Michezo hiyo ya hatua ya 16 awali ilipangwa kuchezwa bila uwepo wa mashabiki lakini uwepo wa vikwazo vya kusafiri baina ya mataifa hayo mawili (Hispania na Italia) vimepelekea kuhairishwa kwa mitanange hiyo.

Uefa wamesema watatolea taarifa ya michezo hiyo kuhusu ratiba mpya.

Roma walishasema kuwa hawatasafi kwenda Sevilla huku naye Rais wa Getafe alisema hawataenda Italia. Pamoja na kauli hizo lakini bado mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Atalanta dhidi ya Valencia siku ya Jumatano uliendelea kama kawaida.

Hofu ya Virusi vya Corona Italia inakuja kipindi hiki ambacho Italia ndiyo nchi inayoongoza kwa kuwa na waathirika wengi mbali na China, waathirika wanaokaribia kufika 10,000.
Michezo mingine iliyokumbwa na kadhia hiyo ni pamoja na ule wa Ligi ya Mabingwa kati ya PSG na Borussia Dortmund utakaochezwa bila mashabiki, Manchester United dhidi ya LASK utakaopigwa bila mashabiki pia. Wakati ule wa Manchester City dhidi ya Arsenal wa Ligi Kuu England uliopagwa kuchezwa leo Jumatano umehairishwa kabisa kuchezwa kutokana na hofu ya Corona.
Chelsea ikiwa ugenini dhidi ya Bayern Munich pia mashabiki hawataweza kuutazama mchezo huo, maombi ya Wolves kusitisha mchezo wao Uefa wamepiga chini.

Ugonjwa wa Corona, unaambukizwa kwa hewa ambapo dalili zake ni kama kukohoa, na kuhema kwa shida, mpaka sasa umeenea kwa kiwango kikubwa ambapo zaidi ya watu 116,000 wameathirika na Virusi hivyo duniani. Wanasayansi wamethibitisha kuwa ugonjwa huo unahitaji siku tano dalili zake kuonekana.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends