Jasho la Greenwood laipa alama tatu muhimu Man United mbele ya Wolves

Manchester United imevuna alama tatu za jasho mbele ya Wolves katika dimba la Molineux mtanange wa Ligi Kuu England uliopigwa Leo Jumapili Agosti 29 kwa kushinda ushindi wa bao 1-0.

Ushindi wa Manchester United umechagizwa na ingizo jipya kutoka Real Madrid mlinzi wa kati Raphael Varane aliyempigia pasi mshambuliaji Mason Greenwood ambaye alikwamisha mpira nyavuni kwa shuti la mguu wa kulia

Cristiano Ronaldo hakuwepo katika dimba la Molineux, lakini mashabiki wa Manchester United ambao walisafiri kuelekea dimba hilo walitumia muda mwingi kuimba jina lake.

United wanaelekea kukamilisha uhamisho wa kumrudisha Ronaldo kwa dau la pauni milioni 12.8, anarejea akiwa mshindi wa Ballon d’Or mara tano.

Bado Ole Gunnar Solskjaer anaendelea kupata shida kwenye kikosi chake kufuatia kushindwa kupata ubora wa wachezaji.

Kama si ubora wa David de Gea pengine, Wolves wangetoka kipindi cha kwanza wakiwa wanaongoza bao 3-0 kwani Raul Jimenez, Trincao na Joao Moutinho walikuwa katika nafasi ya kufunga goli.

Baada ya matokeo hayo, Manchester United wanafikisha pointi saba kwenye nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi Kuu England.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares