Jesse Were aipa Zesco United ushindi katika mechi ya CAF

303

Mshambuliaji Wa kimataifa wa Kenya Jesse Were ameisaidia timu yake ya Zesco United kushinda baada ya kufunga goli mbili katika mchezo dhidi ya klabu ya Sonidep ya Niger katika mashindano ya klabu bingwa Afrika 2018/2019.

Kipyenga cha mwisho cha mwamuzi kiliashiria Zesco United kuibuka na ushindi wa goli 5-1 katika raundi zote mbili za michuano hiyo mikubwa ya pili Afrika. Katika klabu hiyo wakenya wawili mlinzi David Owino na kiungo wa kati Anthony Akumu wanakipiga tangu mwaka 2015.

Wachezaji wote watatu walianza katika mchezo huo kwa upande wa Zesco na ilimchukua dakika moja Jesse Were kufunga goli la kwanza kupitia pasi murua kutoka kwa Enock Sabumukama

Zesco United inayonolewa na Kocha wa zamani wa Yanga SC ya Dar es Salaam George Lwandamina ilionekana kuwa tofauti na imebadilika katika mchezo huo na kuinyanyasa vilivyo safu ya ulinzi ya Sonidep.

Mchezo wa kwanza uliofanyika nchini Niger, Zesco iliibuka kidedea kwa ushindi wa goli 2-1 hivyo walikuwa na matumaini ya kufanya vizuri na ilikuwa hivyo.

Lazarous Kambole aliyefunga bao la ushindi nchini Niger, alifunga goli la pili kunako dakika ya 26 ya mchezo na kufanya kazi kuwa nguvu Zaidi kwa Sonidep. Were alifunga bao lake la pili lamchezo na kumaliza kazi. Matokeo hayo yanaifanya Zesco kusonga mbele katika hatua ya pili ya mtoano kabla ya kuingia kwenye makundi.

Author: Bruce Amani