John Bocco aongeza mkataba Simba

Klabu ya Simba baada ya kukaa kimya tangu kumalizika kwa ligi kuu Tanzania bara na dirisha la usajili kufunguliwa bila kusaini mchezaji yeyote sasa miamba hiyo ya soka imeanza zoezi hilo kwa kumuongezea mkataba nahodha wao John Raphael Bocco.

Mshambuliaji John Raphael Bocco ambaye pia ni nahodha wa kikosi hicho amesaini mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kuichezea Simba kwa miaka miwili leo mbele ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Mohammed Dewji ‘MO’.

Bocco ambaye alikuwa mchezaji bora wa Simba na Ligi Kuu kwa msimu wa 2017/18 na Mshambuliaji Bora kwa msimu wa 2018/19 amefunga jumla ya mabao 30 ya Ligi katika misimu miwili aliyokaa Simba tangu asajiliwe kutoka Azam FC ambako nako aliondoka akiwa mfungaji wa mda wote.

Kuongezwa kwa mkataba kwa Bocco kunakuja kipindi ambacho amekuwa akihusishwa kujiunga na miamba ya soka Afrika ambapo Zamaleck ya Misri na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini zilikuwa zinamhitaji kwa kiasi kikubwa.

Meddie Kagere na Emmanuel Okwi wamekuwa wakihusishwa kuondoka pia Simba baada ya vilabu kutoka Afrika Magharibi kuonyesha nia ya kuwahitaji.

Author: Bruce Amani