Juventus yaweka mkono mmoja kwenye ubingwa wa ligi

Juventus imezima gumzo lote la ushindani kwa udhibiti wao wa ligi kuu ya kandanda Italia – Serie A baada ya kupambana na kupata ushindi wa 2 – 1 dhidi ya Napoli. Ilikuwa mechi kali kati ya vinara wa ligi Juve na nambari mbili Napoli, ambapo kila upande ulishuhudiwa mchezaji wake akipewa kadi nyekundu. Juve sasa wameweka pengo la pointi 16 kileleni.

Hii ina maana kuwa vijana hao wa kocha Massimiliano Allegri ni kama wameweka kibindoni taji lao la nane mfululizo. Mechi hiyo ilikuwa kali hasa baada ya mfungaji bao la Juve Miralem Pjanic kutimuliwa uwanjani kwa kuunawa mpira uliopigwa na Napoli na kulishwa kadi ya pili ya njano baada ya kipindi cha mapumziko.

Kiungo Pjanic alifunga bao la ufunguzi kupitia freekick katika dakika ya 28, ambayo ilipatikana punde tu baada ya Napoli kubaki wachezaji 10 uwanjani wakati kipa yao Alex Meret alimuangusha Cristiano Ronaldo katika eneo la hatari. Emre Can aliongeza la pili kupitia mkwaju wa kona. Napoli walirejea mchezoni kupitia bao la Jose Callejon lakini Juve wakapambana na kuulinda ushindi wao wa 2 – 1.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends