Kagera, Mwadui kucheza katika ligi kuu Tanzania msimu ujao

Michezo ya mtoano ya kuzipata timu mbili zitakazocheza Ligi Kuu ya Tanzania bara msimu wa 2019/20 imechezwa na kupatikana kwa timu hizo baada ya kuchezwa michezo miwili katika viwanja viwili tofauti.

Katika mchezo uliofanyika dimba la Kaitaba, Kagera Sugar wakiwa wenyeji wa Pamba, Kagera wameibuka na ushindi wa goli 2-0.

Mabao ya Ally Ramadhan dakika ya 51 kipindi cha pili na Japhet Makalai katika dakika ya 79 yameiwezesha Kagera Sugar kusalia katika Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Ni kutokana na matokeo ya mechi zote mbili baada ya mtanange wa mkondo wa kwanza uliochezwa Mwanza, ulimalizika kwa sare tasa ya bila kufungana.

Matokeo hayo yanairejesha rasmi Kagera Sugar inayonolewa na Mecky Maxime kunako ligi na itakuwa moja ya timu za msimu mpya ujao wa 2019/20.

Ikumbukwe walima miwa hao wa Kagera waliingia hatua ya mtoano baada ya kumaliza ligi ya msimu huu wakiwa na alama 44 katika nafasi ya 18 ya msimamo wa ligi.

Mbali na Kagera kusalia, Mwadui FC kutoka Kishapu, Shinyanga nayo imesalia katika ligi kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Geita Gold Mine.

Ushindi huo umepatikana kupitia mabao ya Salim Aiyee aliyeingia kambani mara mbili kunako dakika za 33 na 90+3 huku bao pekee la Geita likifungwa na Baraka Jerome katika dakika ya 50.

Kupoteza kwa Geita Gold kunawafanya waungane na Pamba kuendelea kusalia Ligi Daraja la Kwanza kwa ajili ya kupambania nafasi nyingine tena ya kusaka tiketi ya kupanda Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao.

Author: Asifiwe Mbembela