Kahata ahaimia rasmi Simba kutoka Gor Mahia

Kiungo wa Kimataifa wa Kenya Francis Kahata Nyambura amejiunga na Simba Sports Club kwa kandarasi ya miaka miwili akitokea mabingwa wa Kenya, Gor Mahia.

 

Kahata, 27, amejiunga na Simba baada ya mkataba aliousaini na Gor Mahia mwaka 2015 kumalizika Julai Mosi mwaka huu hivyo Simba imemchukua kama mchezaji huru licha ya malipo kwa mchezaji husika kutajwa kama milioni 80 za Kitanzania.

Usajili wa Simba kwa Kahata unakuja kipindi ambacho Simba imeachana na viungo wawili James Kotei na Haruna Niyozima huku Mkenya huyo akiwa na uwezo wa kutimiza vyema majukumu katika nafasi mbili, kiungo mkabaji, na kiungo mshambuliaji muda mwingi hata kusimama nyuma ya straika.

Kahata alikuwa katika kiwango bora kwa misimu mitatu mfululizo huku msimu 2018/2019 ukiwa bora zaidi, jambo ambalo lilimshawishi kocha wa timu ya taifa “Harambee Stars” Sebastian Migne kumjumuisha kwenye kikosi cha mwisho cha wachezaji walioenda kushiriki Afcon 2019 Misri.

Kiungo huyo anaungana tena na mshambuliaji Meddie Kagere Simba baada ya wachezaji wote wawili kukipiga Gor Mahia kabla ya Kagere kutimukia kwa Wekundu wa Msimbazi Simba na sasa wako pamoja.

Author: Asifiwe Mbembela

Facebook Comments