Kaizer Chiefs yatoa kipigo kizito kwa Simba, Gomes aduwazwa

Kocha Mkuu wa Simba Didier Gomes Da Rosa ameduwazwa na kipigo cha goli 4-0 kutoka kwa Kaizer Chiefs katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali mkondo wa kwanza uliopigwa katika dimba la Soccer City nchini Afrika Kusini.

Simba ambayo ilifika hatua ya robo fainali baada ya kuongoza kwenye Kundi A lililokuwa na Al Ahly, AS Vita, EL Merreikh ilikuwa na matumaini ya kufanya vizuri kutokana na takwimu za michezo ya hatua ya makundi lakini mambo yalianza kuwa tofauti dakika ya 6 ya mchezo.
Kufuatia Eric Mathoto kukwamisha mpira nyavuni akimalizia mpira wa kona ambao walinzi wa Simba walishindwa kukaba kwa wakati.
Dakika chache tena baada ya goli la kwanza, Kaizer Chiefs ambao wanamilikiwa na Bosi Kaizer walipata bao la pili kupitia kwa mshambuliaji wa timu hiyo Samir Nurkovic akifunga kwa kichwa kufuatia mlinzi Shomari Kapombe kushindwa kufanya ukabaji mzuri.
Mpaka filimbi ya mwamuzi kuashiria mapumziko Simba walikuwa nyuma kwa bao 2-0.
Hata hivyo, kama wasemavyo waswahili kuwa ngoma ya watoto haikeshi, Kaizer wakaingia kambani kwa kufunga goli la tatu dakika ya 57 Nurkovic akitumia makosa ya beki Mohammed Hussein na bao la mwisho likifungwa na Castro Leonardo Casro.
Inakuwa mara ya kwanza kwa kocha Didier Gomes kufungwa goli zaidi ya moja ndani ya kikosi cha Simba kwenye michuano hiyo, sawa na kwa kipa Aishi Manula ambaye alikuwa hajaruhusu bao hizo.
Sasa kazi inabaki Mei 22 kwa Mkapa ambapo Simba watakuwa wanasaka ushindi wa mabao matano bila kuruhusu kufungwa ili waweze kutinga hatua ya nusu fainali.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares