Kariobangi Sharks mabingwa wapya wa SportPesa Cup

108

Klabu ya Kariobangi Sharks imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Sportpesa SuperCup 2019 kwa mara ya kwanza baada ya kuifumua Bandari FC zote kutoka Kenya kwa goli 1-0 katika mchezo uliopigwa katika dimba la taifa jijini Dar es Salaam ambapo mashindano hayo yalikuwa yanafanyika.

Kariobangi walionekana kuzidiwa katika kipindi cha kwanza hasa kutokana na kasi waliyoingia nayo Bandari wakishambulia kwa kasi na kupiga mashuti ya mbali.

Kipindi cha pili kilikuwa na neema kwa Sharks baada ya kufanikiwa kupata goli moja kunako dakika ya 60 kupitia kwa Mwenda Harrison baada ya walinzi kushindwa kuondosha mpira uliokuwa ukielekea langoni kwao.

Matokeo hayo yanaifanya Kariobangi Sharks kutwaa ubingwa wa Sportpesa SuperCup kwa mara ya kwanza baada ya miaka miwili ya utawala wa Gor Mahia ambayo ilichukua ubingwa huo mara mbili mfululizo 2017/18 na 2018/19.

Bandari FC haina historia kubwa sana katika Ligi kuu nchini Kenya wala Sportpesa ingawa imeleta upinzani mkubwa katika michuano ya mwaka huu sawa na Mbao FC.

Kariobangi Sharks wamejinyakulia zaidi ya kitita cha milioni 60 za Kitanzania sambamba na kucheza na Everton kutoka England, mchezo huo utafanyika nchini Kenya.

Sharks wamekabidhiwa taji na Steven Pinner ambaye ni balozi wa Kampuni hiyo ya michezo ya kubahatisha.

Author: Bruce Amani