Kassim Majaliwa aongeza hamasa mechi ya Namungo dhidi ya Yanga

Mabingwa wa kihistoria (27) Yanga watashuka dimba la Kassim Majaliwa kukwaruzana dhidi ya Namungo FC mchezo wa Ligi Kuu Vodacom Tanzania bara raundi ya pili, mtanange utakaofanyika kesho Jumapili majira ya saa 10 jioni.

Yanga itaingia katika mchezo huo wakitoka kupoteza mchezo uliopita dhidi ya KMC baada ya kukubali kichapo cha goli 1-0, goli la Salum Aiyee ambapo kabla ya mchezo huo pia walitoka kushinda Kariakoo dabi 1-0 Simba.

Wakati Namungo wakiwa wapo kwenye msimu wa kwanza tangu wamepanda Ligi Kuu wataingia wakiwa wanahitaji kuendelea kuipa hofu Yanga katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa VPL ambapo hivi sasa inakamata nafasi ya nne wakiwa na alama 49 tofauti ya alama moja na Yanga walio nafasi ya tatu.

Kuelekea mchezo huo, Waziri Mkuu wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa, Kassim Majaliwa ametoa hamasa kwa wakazi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi kuipa nguvu Namungo FC kwenye mchezo wao dhidi ya Yanga SC,

“Kesho tunakwenda kumparua mtu mzima”

Hamasa hiyo huenda ikawapa nguvu zaidi Namungo ambayo imekuwa na matokeo mazuri zaidi kwenye uwanja wa nyumbani kuliko ugenini huku wakitegemea ubora wa Bigirimana Blaise, Lusajo na wengineo. Matokeo ya mchezo huo huenda yasiwe na maana sana katika mbio za ubingwa zaidi ya kulinda heshima sambamba na kuendelea katika nafasi wanazozikamata kwa sasa.

Michezo ya leo Jumamosi VPL

Singida United 2-1 Mbeya City

Lipuli 0-1 Kagera Sugar

Mtibwa Sugar 1-1 Biashara United

Polisi Tanzania 1-0 Ndanda

Mwadui 2-1 Tanzania Prisons

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends