Kenya mabingwa wa Kombe la Cecafa Wanawake 2019

327

Timu ya kandanda ya wanawake ya Kenya Harambee Starlets ndio washindi wa Kombe la Cecafa 2019.

Starlets waliwafunga Kilimanjaro Queens wa Tanzania mabao 2 – 0 katika fainali ya Jumatatu kwenye uwanja wa Chamazi, mjini Dar es Salaam na kubeba taji lao la kwanza la kikanda.

Kenya walilipiza kisasi kichapo cha 2 – 1 kwa Tanzania katika fainali ya 2016 mjini Gulu, Uganda.  Kenya imebeba kombe hilo na rekodi ya kutoshindwa mechi yoyote na bila kufungwa bao katika mashindano hayo.

Uganda waliwafunga Burundi 2 – 0 katika mtanange wa kumtafuta mshindi wa medali ya shaba.

Wakati huo huo, timu ya wanaume Harambee Stars watafufua tena uhasama wao na timu Taifa Stars ya Tanzania wakati wakilenga kutetea taji lao la Cecafa Senior Challenge mwezi ujao nchini Uganda.

Timu hizo mbili zimepangwa katika Kundi C pamoja na Zanzibar na Djibouti. Dimba hilo litaanza Desemba 7 hadi 19.

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo watashiriki kama wageni, na wamepangwa pamoja na Sudan, Sudan Kusini na Somalia

Wenyeji Uganda wako katika Kundi A pamoja na Burundi, Ethiopia na Eritrea.

Author: Bruce Amani