Kikosi cha Kenya cha Afcon chazusha minung’uniko

Kocha wa timu ya taifa ya soka ya Kenya Mfaransa Sebastien Migne amekitaja kikosi cha awali cha wachezaji 27, kuelekea fainali ya mataifa bingwa barani Afrika, itakayoanza mwezi ujao nchini Misri.

Migne amemwacha nje ya kikosi hicho mshambuliaji mkongwe na wa siku nyingi Allan Wanga, anayechezea klabu ya Kakamega Homeboyz katika ligi kuu ya Kenya nchini humo.

Wapenzi wa soka nchini humo kupitia mitandao ya kijamii, wameonekana kushangazwa na kuachwa nje kwa Wanga ambaye ni miongoni mwa washambuliaji waliofanya vyema katika ligi kuu ya soka nchini humo.

Wachezaji wengine waliotemwa ni pamoja na kiungo wa kati ya Whyvonne Isuza wa AFC Leopards na kipa wa klabu ya Kariobangi Sharks Brian Bwire.

Harambee Stars ambayo imepangwa pamoja na Tanzania, Senegal na Algeria katika michuano hiyo ya AFCON itakwenda Ufaransa kwa ajili ya maandalizi ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika.

Author: Bruce Amani