Kinyang’anyiro cha Bundesliga chazidi kupamba moto

Ligi Kuu ya Ujerumani inazidi kupamba moto na Bayern Munich sasa wako pointi moja tu nyuma ya vinara RB Leipzig. Hii ni baada ya Bayern kupata ushindi mkubwa wa magoli matano kwa bila dhidi ya Schalke uwanjani Allianz Arena katika wakati ambapo RB Leipzig walikuwa ugenini wakicheza na Eintracht Frankfurt na wakalazwa kwa magoli mawili bila jawabu.

Sasa baada ya matokeo hayo Leipzig wana pointi arubaini kileleni baada ya mechi kumi na tisa na Bayern Munich pointi zao ni thelathini na tisa kisha walio kwenye nafasi ya tatu ni Borussia Moenchengladbach ambao wana pointi thelathini na nane. Nafasi ya nne inashikiliwa na Borussia Dortmund wakiwa na pointi thelathini na sita kisha tano bora inafungwa na Bayer Leverkusen ambao wanajivunia pointi thelathini na nne baada ya ule ushindi wao wa tatu bila jana walipocheza na Fortuna Dusseldorf.

Mkiani kuna Werder Bremen ambao nafasi yao ya kumi na sita wakiwa pointi kumi na saba halafu Paderborn wanawafuata wakiwa na pointi kumi na tano na wanaouvuta mkia ni Fortund Dusseldorf wenye pointi kumi na tano pia sawa na Paderborn ila wanadunishwa na uchache wa magoli ndio maana wako chini ya jedwali.

Author: Bruce Amani