Kipa wa Bayern Manuel Neuer arefusha mkataba na mabingwa hao wa Ujerumani hadi 2023

Mlinda lango wa timu ya taifa ya Ujerumani, Manuel Neuer, ameongeza kandarasi yake katika klabu ya Bayern Munich kwa miaka miwili na sasa atasalia katika klabu hiyo hadi Juni mwaka 2023.

Neuer mwenye umri wa miaka 34 na ambaye ni nahodha wa Bayern, kwa muda mrefu amekuwa akifanya mazungumzo na klabu hiyo hasa baada ya Bayern kumsajili yule anayeonekana kuwa atakayeichukua nafasi yake kuanzia msimu ujao, Alexander Nubel kutoka Schalke.

Lakini mazungumzo ya kumuhakikishia Neuer nafasi yake katika klabu hiyo yalizaa matunda huku mabingwa hao wa Bundesliga wakitangaza nyota huyo atasalia kuwa mmoja wa hao Bavarias.

“Kwa urahisi sana naweza kujiweka katika hali ambayo Neuer yuko sasa hivi,” alisema Oliver Kahn, mlinda lango wa zamani wa Bayern Munich. “Tunaelewa mwelekeo anaotaka kuchukua Manuel katika kipindi hiki cha taaluma yake na kile kilicho muhimu kwake. Ametuma ujumbe mzito na nyongeza hii ya kandarasi,” aliongeza Kahn.

Neuer ambaye alishinda Kombe la Dunia na Ujerumani mwaka 2014 alijiunga na Bayern kutoka Schalke mwaka 2011 na alichaguliwa kama mlinda lango bora duniani mara nne. Ameshinda mataji saba yaliyopita ya Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga na Bayern Munich, pamoja na mataji matano ya Kombe la Shirikisho na ile Ligi ya Vilabu Bingwa Barani Ulaya mwaka 2013.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends