Kipchoge aivunja rekodi yake ya ulimwengu ya marathon Berlin
Mashabiki waliokusanyika asubuhi katika mitaa ya mapema walimpa morali na msukumo wa kutaka avunje rekodi aliyoiweka yeye mwenyewe miaka minne iliyopita. Na hilo alilifanikisha kwa uzuri kabisa. Mpaka sasa hakuna anayebisha kuwa Eliud Kipchoge, ndiye mfalme wa mbio za marathon ulimwenguni. Mkenya hiyo ameshinda mbio za marathon za Berlin kwa kuandikisha muda wa masaa mawili, dakika moja na sekunde tisa.
Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 37 alipunguza kwa sekunde 30 muda aliouweka katika mwaka wa 2018 hapo katika mji huo mkuu wa Ujerumani. Sasa ameshinda mbio 15 za marathon kati ya 17 katika Maisha yake, ukiwemo ubingwa mara mbili wa Olimpiki na mataji 10 makuu.
Muethiopia Tigist Assefa alishinda mbio za wanawake kwa kutumia muda wa masaa mawili, dakika 15 na sekunde 37. Alipunguza kwa dakika 18 muda bora aliowahi kuandikisha kabla. Huo ndio muda wa tatu wa kasi Zaidi kuwahi kuwekwa katika mbio za marathon za wanaume.
Kichoge alimaliza karibu dakika tano mbele ya Mkenya mwenzake Mark Korir, aliyemaliza katika nafasi ya pili kwa muda wa masaa mawili, dakika tanon na sekunde 58. Muethiopia Tadu Abate alimaliza katika nafasi ya tatu na muda wa masaa mawili dakika sita na sekunde 28.
Kabla ya mbio hizo, Kipchoge aliiambia BBC kuwa hawezi kutabiri kitakachofanyika Berlin lakini lengo lake lilikuwa ni kuwa na mbio nzuri.
“Kama kila kitu kitaenda sawa na uwe muda bora kwangu au rekodi ya ulimwengu, basi nitasherehekea.” Sijui ukomo wangu, hasa, mjini Berlin. Lakini nitajribu kujisukuma. Sijui ukomo uko wapi.”
