Klopp apagawa na kipigo cha Real Madrid Ligi ya Mabingwa

Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp amesema timu yake haikujituma vya kutosha kiasi cha kuruhusu kupigwa goli 3-1 na mabingwa mara 13 wa Ligi ya Mabingwa Ulaya Real Madrid mchezo wa robo fainali mkondo wa kwanza uliopigwa dimba la Santiago Bernabeu Jumanne Aprili 6.

Liverpool ambao wako kwenye hali mbaya ndani ya EPL kutokana na matokeo yasiyo na mwendelezo mzuri, walijikuta wako nyuma kwa bao moja baada ya winga wa Madrid Vinicius Junior kukwamisha mpira nyavuni akimalizia mpira wa kiungo wa Ujerumani Toni Kroos.

Marco Asensio aliongeza bao la pili kabla ya mapumziko na kufanya matokeo kuwa 2-0, Asensio alifunga goli hilo kwa makosa ya beki wa kulia wa Majogoo wa Jiji la Merseyside Trent Alexander-Arnold.

Liverpool waliingia kipindi cha pili kwa nguvu wakafanikiwa kupata goli kupitia kwa Mohammed Salah lakini Vinicius alikuwa “supa” kwenye mechi hiyo akaongeza bao la tatu dakika 25 kabla ya kipyenga cha mwamuzi.

Mchezo wa marudiano utachezwa Aprili 14 kwenye dimba la Anfield ambalo litakuwa bila mashabiki kutokana na taadhali ya virusi vya Corona.

“Kama unahitaji kufika nusu fainali, fainali lazima utoe kilichobora, hatukufanyi hivyo sisi (Liverpool).

“Hatukucheza vizuri kiasi cha kuwa sababishia matatizo Real Madrid, tulikuwa rahisi sana kwao”.

“Tumecheza dakika 45 za kwanza, kuna dakika 45 nyingine nyumbani, tunaenda kujipanga”.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares