KMC yalamba pesa za M-Bet kabla ya kuivaa AS Kigali

Klabu ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni – KMC imeingia kwenye mkataba wa miaka mitano na Kampuni ya M-Bet kwa ajili ya kuidhamini timu hiyo katika kutengeneza vifaa vya timu hiyo kandarasi yenye thamani ya bilioni moja.

KMC inayoshiriki michuano ya Kimataifa kwenye Kombe la Shirikisho imeingia kwenye mkataba huo kwa mara ya kwanza tangu klabu hiyo kupanda daraja msimu wa 2016/2017 na kisha kukamata nafasi ya nne katika msimamo wa TPL.

Akizungumza na Waandishi wa habari, Meneja Masoko wa M-Bet, Allen Mushi amesema kuwa wameamua kuichagua KMC kati ya timu 20 ambazo zinashiriki Ligi Kuu Bara kutokana na mafanikio ambayo wameyapata kwa muda mfupi.

“M-bet tumeichagua KMC kutokana na namna ambavyo imejipambanua vema katika sekta ya mpira baada ya kupanda daraja ilikuwa ikifanya vema na imeleta ushindani mkubwa.

Mwenyekiti wa bodi ya KMC, Benjamin Sitta amesema kuwa: “M-bet ni kampuni maalumu ya michezo ya kubashiri na tumeingia nao mkataba wa miaka mitano wenye thamani ya bilioni moja.

Mkataba wa KMC unakuja kipindi ambacho Ligi Kuu ya Tanzania bado haina mdhamini mkuu hivyo inakuwa ni neema kubwa kwa klabu hiyo baada ya msimu uliopita kupitia changamoto lukuki.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends