Kocha Desabre akalia kuti kavu Wydad Casablanca

Kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Uganda na Pyramids ya Misri Sebastien Desabre anakabiliwa na shinikizo na huenda akafutwa kazi katika klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco baada ya mwendelezo mbovu wa matokeo ndani ya Ligi pamoja na michuano ya CAF.

Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa kocha huyo wa zamani wa Ismaili ya Misri pia huenda akajiunga na mabingwa mara mbili wa AFCON Ivory Coast inayojaribu kutafuta nafasi ya kufuzu mashindano ya fainali za Kombe la Dunia Qatar 2022 na Kombe la Mataifa Afrika AFCON 2021.

Huku ripoti nyingine zimekuwa zikieleza kuwa baada ya kikao kilichofanyika baina ya pande mbili walikubaliana kwamba kocha Desabre ataendelea kushikilia kijiti hicho mpaka kocha mpya atakapopatikana.

Lakini baada ya kipigo cha wiki iliyopita kutoka kwa timu inayokamata nafasi ya 19 kwenye msimamo wa Ligi ya  Botola, Youssoufia Simba wa Afrika wamebadilisha mawazo na wanataka aondoke mapema kabla ya mchezo wao dhidi ya Etoile du Sahel.

Wydad Casablanca wapo alama moja juu ya RS Berkane baada ya michezo 17 ya ligi hiyo huku wakiwa wamecheza michezo mitano bila kushinda hata mmoja, pia wapo hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo watacheza na miamba ya Tunisia Etoile du Sahel mkondo wa kwanza Jumamosi ya tarehe 29, 2020.

Amani sports news inatambua kuwa kocha wa Kihispania na kocha wa zamani wa Etoile du Sahel na Raja Juan Carlos yuko mbioni kuchukua mikoba ya Mfaransa Sebastien Desabre.

Desabre alijiunga na Wydad Casablanca mwezi Januari 2020 kwa kandarasi ya miaka miwili na nusu ambapo ametumikia miezi miwili pekee kutoka kwenye mkataba wake.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends