Mourinho akalia kuti kavu Tottenham, achapwa 2-1 na West Ham United

West Ham imekwea mpaka nafasi ya nne katika msimamo wa EPL kwa kupata alama tatu mbele ya Tottenham Hotspur baada ya kuandikisha ushindi wa goli 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu nchini England mtanange uliopigwa leo Jumapili.

Ushindi wa West Ham United unaongeza hofu na presha zaidi kwa kocha Jose Mourinho ambaye wiki hii kulikuwa na tetesi kuwa kocha wa Leicester City Brendan Rodgers anawaniwa kuchukua mikoba yake.

Wagonga Nyundo wa London walianza kutangulia kupata goli kupitia kwa Michail Antonio ambaye unakuwa mchezo wake wa kwanza kufuatia kukosa mechi mbili baada ya mlinda mlango Hugo Lloris kushindwa kuudhibiti mpira wa Jarrod Bowen.

Goli la pili la West Ham United limefungwa na kiungo mshambuliaji wa Manchester United ambaye anakipiga kunako klabu hiyo kwa mkopo Jesse Lingard na kufanya 2-0.

Gareth Bale aliyeingia kama mchezaji wa akiba alisaidia kupatikana kwa goli baada ya kusaidia upatikanaji wa bao la Lucas Moura.

Ushindi kwa kocha David Moyes dhidi ya kocha Jose Mourinho unakuwa wa kwanza katika mechi 16 zilizopita, West Ham wanapanda mpaka nafasi ya nne alama mbili mbele ya Chelsea walionafasi ya tano na Spurs wapo nafasi ya tisa.

Author: Bruce Amani

Sharing is caring!

0Shares