Kocha Nkata afungiwa mfereji Kakamega

AMEKUA akiishi katikati ya kaunti ya Kakamega kwa miezi tisa sasa. Iwapo hufahamu Kakamega, huu ni mojawapo miji bora nchini Kenya pongezi kwa juhudi za Gavana Wycliffe Ambetsa Oparanya.

Kwa habari Zaidi kuhusu kaunti hii, kaitembelee mwenyewe maana kwa sasa tunazungumzia spoti ambapo kocha wa Kakamega Homeboyz Paul Nkata amefutwa kazi baada ya kusemekana amekua akipanga matokeo ya mechi na baadhi ya wachezaji.

Mwenyekiti wa Homeboyz Cleophas Shimanyula alidai kocha huyu Mganda amekuwa akiwapa baadhi ya wachezaji kati ya laki moja na mbili ili kupanga matokeo.

“Mechi dhidi ya Sony Sugar ambayo tulipoteza 2-1 beki wetu akijifunga bao kisha baina ya Mathare United tukipigwa 3-2 ni baadhi ya zile tumepata ushuhuda kwamba walishirikiana kupanga,” alisema Shimanyula.

“Tumemtuma nyumbani yeye pamoja na naibu wake Hamza Kalanzi na kiungo George Mandela tukiendelea kufanya uchunguzi. Tumefahamisha FKF ichukue hatua swala hili nzito ambalo linaharibu soka letu,” aliongeza.

Straika wa Harambee Stars Allan Wanga na kocha wa makipa David Juma wamepewa majukumu ya kuongoza timu hiyo kwa muda.

Watasaidiwa na mwelekezi wa kiufundi Eliud Omukuyia.

Kwa Nkata, iwapo ni kweli amekua akipokea mamilioni ya hela kutoka nje ili kugawana na wachezaji kupanga mechi, basi mfereji wake wa chapaa umefungwa na Shimanyula.

Nyota huyu wa zamani wa timu ya Uganda Cranes amewahi kufunza vilabu vya City Stars, Muhoroni Youth, Tusker na Bandari.

Alishinda taji la ligi kuu na la Ngao ya GOtv mwaka 2016 akiwa Tusker.

Author: Bruce Amani

Facebook Comments