Kocha Pablo wa Simba aomba muda zaidi

Kocha mkuu wa klabu ya Simba Sc, Pablo Franco amesema ili kuiunda timu shindani katika makombe ya ndani na nje ya Tanzania anahitaji muda zaidi wa kuisoma Simba, wachezaji na soka lenyewe la nchini hapa.

Simba ambao ndiyo mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikishi ‘ASFC’ wanakibarua kizito kwenye michuano ya Afrika Kombe la Shirikisho dhidi ya Red Arrows ya Zambia na kutetea taji la Ligi na Shirikisho la ndani.

Pablo amesema tangu aanze majukumu ya kuifundisha timu hiyo ameshuhudia vipaji vya hali ya juu kwa wachezaji wake.

“Nafurahi kuona kazi yangu haitakuwa ngumu sana kutokana na uwezo walionao wachezaji niliowakuta hapa, bado nasubiri wale waliopo timu ya taifa nadhani wiki tatu zitatosha kutufanya kuwa bora,” amesema Pablo.

Amesema anajua falsafa ya klabu ya Simba ni kupiga pasi nyingi, na hilo anataka kuliongezea vitu ili liweze kunoga na kuwachanganya wapinzani wao kitu ambacho kitawasaidia kupata ushindi kirahisi.

Pablo amejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akichukua mikoba ya Kocha kutoka nchinin Ufaransa Didier Gomes ambaye aliamua kuachia ngazi baada ya klabu hiyo kushindwa kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa na Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Mchezo wa kwanza kwa kocha huyo utakuwa dhidi ya Ruvu Shooting wikiendi hii Jijini Mwanza.

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends