Kocha Sven Vandenbroeck afutwa kazi Simba

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini Tanzania klabu ya Simba wametangaza rasmi kuwa wameachana rasmi na aliyekuwa kocha wa timu hiyo Sven Vandenbroeck kwa kile walichokieleza kuwa ni makubaliano ya pande mbili.

Hii ikiwa ni siku moja baada ya Simba kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Mabingwa Afrika kwa ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya FC Platinum kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Januari 6.

Simba ilipoteza mchezo wa kwanza ugenini, Uwanja wa Taifa wa Zimbabwe kwa kufungwa bao 1-0 ila ushindi walioupata jana Uwanja wa Mkapa wa mabao 4-0 umewafanya wasonge mbele kwa jumla ya idadi ya mabao 4-1.

Sven alipokea mikoba ya Patrick Aussems ambaye alifutwa kazi kwa kushindwa kuifikisha timu hiyo hatua ya makundi baada ya kutolewa na UD Songo kwenye hatua ya awali.

Kocha msaidizi Seleman Matola aliyekuwa kwenye majukumu ya timu ya taifa amerudishwa katika majukumu ya klabu hiyo ambayo ipo visiwani Zanzibar kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares