Kocha wa Arsenal, Arteta asema Man City ni timu bora Ulaya

Ni ajabu kidogo. Ni jambo ambalo ni gumu kulisema na kuliweka wazi kama utakuwa na roho ya korosho. Ukishakuwa mnafiki hili hauwezi kuliweka bayana hata siku moja. Kuna mtani mmoja wa soka anasema “Shabiki, mdau aliyekunywa rangi ya jezi hawezi kusema hivyo” lakini kocha wa Arsenal Mikel Arteta amelisema hadharani bila uficho.

Hutokea baadhi ya nyakati kauli kama hizo hutolewa kinafiki, lakini hii imetoka kwenye kinywa cha kocha ambaye hana sifa ya uongeaji wa hivyo. Ingekuwa ni Jose Mourinho amesema ni rahisi kuamini kuwa huenda unafiki upo lakini ni Arteta.

Arteta anasema inawezekana Manchester City ni timu bora Ulaya kwa sasa.

City walichukua uongozi wa EPL kwa tofauti ya alama 10 baada ya ushindi wa katikati ya juma dhidi ya Everton, na bado wameingia fainali ya Carabao, wapo FA na bado wanashindania taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya..

Kikosi cha kocha Arteta kitacheza dhidi ya Manchester City Jumapili, akisema “ni kazi ngumu kukutana na City lakini utakuwa mchezo mzuri”.

City imepoteza michezo miwili tu katika mechi 24 za mwanzo, walipoteza dhidi ya Leicester City mwezi Septemba na Tottenham mwezi Novemba.

“Nafikiria ni timu bora kwa sasa barani Ulaya”.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares