Kocha wa Ausgburg Heiko Herrlich kukosa mechi dhidi ya Wolfsburg kwa kukiuka hatua za kukaa karantini

Kocha mkuu wa timu ya soka ya Augsburg Heiko Herrlich atakosa mechi yake ya kwanza kutokana na kukiuka sheria za kukaa karantini kabla ya kuanza tena kwa mechi za Bundesliga.

Ijumaa (15.05.2020) wachezaji wa Augsburg walikuwa wakifanya mazoezi bila kocha Herrlich baada ya kukiuka sheria kali ya kuwekewa karantini ambayo imemuweka nje kuelekea mechi ya kuanza tena kwa Bundesliga dhidi ya Wolfsburg, baada ya ligi hiyo kusimamishwa kwa muda ikiwa ni juhudi za kuepusha kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Corona

Herrlich, aliyeteuliwa siku tatu tu kabla ya ligi kusimamishwa katikati ya mwezi Machi kufuatia mripuko wa janga la virusi vya Corona, aliuambia mkutano wa waandishi wa habari Alhamisi tarehe 14.05.2020 kwamba aliondoka hotelini ambako timu yake imepiga kambi kwenda kununua mswaki na mafuta maalumu ya ngozi.

Lakini kutokana na hatua madhubuti za kuwekwa karantini kwa timu zote kuelekea kuanza tena kwa Bundesliga, kuingia kwake ndani ya duka hata akiwa amevaa barakoa inamaanisha yeye atakosa mchezo wake wa kwanza Jumamosi na hawezi kurudi kufundisha timu hadi pale atakapopima mara mbili virusi vya homa ya corona na kukutikana hana maambukizi.

Alhamisi (14.05.2020) Herrlich aliomba radhi katika taarifa iliyotolewa kupitia kilabu yake, akisema kuwa hatasimamia timu hata kabla ya bodi ya ligi ya soka ya Ujerumani, (DFL) ingekuwa na uwezekano wa kuweka vikwazo sawa.

“Nilifanya makosa kuondoka katika hoteli hiyo. Hata ingawa niliona hatua za usafi hotelini na hivyo, siwezi kutengua hatua hii. Katika hali hii, sikufanya kama mfano wa kuigwa kwangu, timu na umma,” alisema.

Author: Bruce Amani