Kocha wa Manchester United Ole Gunnar ashindwa kutaja golikipa namba moja wa timu

528

Pazia la Ligi Kuu nchini England kwa klabu ya Manchester United linafunguliwa rasmi Jumamosi ambapo Mashetani Wekundu watakuwa dimba la nyumbani Old Trafford kumenyana vikali dhidi ya Crystal Palace majira ya saa 7:30 jioni.

Wakati pazia hilo likifunguliwa kwa United, Kocha wa kikosi hicho ameshindwa kuweka bayana ni nani atakuwa mlinda mlango wake namba moja kwa msimu ujao, lakini pia ni nani atakayeanza katika mtanange wa kesho.

Manchester United wana magolikipa watatu bora ambao wote ni sehemu ya vikosi vya timu za taifa, wana kipa aliyekuwa kwa mkopo wa misimu miwili Sheffield United Dean Henderson ambaye amekuwa akiitwa timu ya taifa ya England.

Wana mlinda mlango namba moja wa Argentina Sergio Romero ambaye kwa misimu kadhaa iliyopita amekuwa kama kipa msaidizi/namba mbili wa Manchester United.

Namba tatu ni kipa wa timu ya taifa ya Hispania David de Gea ambaye msimu uliopita alikuwa na msimu mbovu baadhi ya nyakati ndani ya uzi wa United.

Sasa kuelekea mtanange wa kesho Meneja wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer amesema “hawezi kusema leo (Ijumaa) kuwa ni nani atakaye anza, lakini magolikipa wote wamekuwa na wakati mzuri wa katika viwanja vya mazoezi, ina nifurahisha”.

“Wapo katika ubora wao, najua makocha wa magolikipa wanafurahia kuwaona wakiwa kwenye ubora wao”.

“Ilikuwa vizuri sana pale ambapo kocha Luis Enrique alisema kichanya juu ya kiwango cha David de Gea katika majukumu ya timu ya taifa, unapozungumza hivyo inasaidia kumpa kujiamini mlinda mlango”

“Lakini mpaka sasa kipa wetu wa Argentina hajarudi lakini amekuwa bora sana”

Licha ya kusifia kuwa walinda mlango wote bora na wanafanya mazoezi kwa juhudi kubwa bado hajaweka wazi ni nani atakuwa mlinda mlango wake katika kikosi cha kwanza.

Mapungufu ya David de Gea msimu uliopita hasa ndiyo yanayoibua maswali kama kocha Solskjaer ataendelea kumuamini na kumpa nafasi ya kuwa kipa namba moja.

Swali ngumu ni Je, atakuwa David, Romero au Henderson ambaye atakuwa namba moja? Ni kesho Manchester United Vs Crystal Palace.

Author: Asifiwe Mbembela