Kocha wa Roma apata muda wa kupumua baada ya ushindi

AS Roma imefanikiwa kuibuika na ushindi wa goli 3-2 katika mchezo mgumu dhidi ya Genoa ikiwa ni mikiki ya  Serie A uliochezwa kwenye dimba la Stadio Olimpico Jumapili ya Disemba 16 na kuendelea kumpa matumaini ya kibarua  kocha Eusebio Di Francesco.

Matokeo hayo yamehitimisha michezo mitano bila kupata ushindi kwa Roma, huku mara ya mwisho kushinda ilikuwa Novemba 11 walipoitandika Sampdoria goli 4-1. Ushindi huo umeisogeza klabu ya Roma katika nafasi ya sita na tofauti ya alama mbili nyuma ya AC  Milan.

Mchezo ya mapema Napoli iliibamiza Cagliari 1-0 na kuendeleza tofauti ya alama nane nyuma ya vinara Juventus ambao pia walipata ushindi kama huo dhidi ya Torino kupitia penati ya Cristiano Ronaldo.

“Ninawashukuru vijana kwa namna ambavyo wamecheza kwenye mazingira magumu namna hii, haikuwa rahisi hata kidogo kwao” alisema Kocha Di Francesco. “Timu bado haiko sawa, niliona heshima na kutamani kurudi nyumbani na alama tatu ambazo tumezipata” aliongeza Di Francesco. 

Cagliari ipo nafasi ya 13 katika msimamo wa Serie A na umekuwa mchezo wa kwanza kupoteza nyumbani kwa timu hiyo. Fiorentina imemaliza ukame wa kutoshinda mchezo baada ya kutoka nyuma na kushinda  goli 3-1 dhidi ya Empoli na sasa wamebakiza alama nne kuingia nafasi 4 za juu ambapo Milan inashikilia kwa alama 26.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends