Kocha wa Valencia Garcia atupiwa virago

Baada ya takribani miezi 10 klabu ya Valencia inayoshiriki Ligi Kuu nchini Hispania – La Liga imemfuta kazi ya ukocha, Javi Gracia Leo Jumatatu kufuatia matokeo mabovu.

Jumapili ya Mei 2, Valencia walikuwa na mchezo dhidi ya Barcelona ambao ulimalizika kwa kipigo kwao cha goli 3-2 ambao ulikuwa mchezo wa mwisho kwa kocha Garcia. Valencia imebakiza alama sita kuangukia kwenye mstari wa kushuka daraja.

Kocha huyo wa zamani wa Watford anaondoka klabuni hapo akiwa ameshinda mechi nane pekee msimu huu.

“Tunakushukuru sana kocha (Garcia) kwa kazi yako kipindi chote ulichokuwa hapa, tunakutakia kila lenye heri kwao” ilisomeka taarifa ya klabu kwa umma.

Washindi hao mara sita wa La Liga kwa sasa wanakamata nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi, mechi nne zimesalia kumalizika kwa kandanda ya La Liga.

Kocha msaidizi Salvador Gonzalez ‘Voro’ atachukua majukumu kwenye mechi zilizobakia.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares