Kocha Yanga atetea sare ya 1-1 na KMC, asema mambo bado!

286

Baada ya mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu nchini Tanzania klabu ya Yanga kubanwa mbavu na kikosi cha KMC kwa sare ya goli 1-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya VPL, kocha wa Yanga asema hawakutumia vyema nafasi ingawa bado ubingwa uko wazi.

Kaimu Kocha Mkuu wa Klabu ya Yanga Juma Mwambusi amesema kuwa sare waliyopata jana haikuwa kwenye mpango wao ila kwa kuwa wamepata pointi moja basi ni jambo la kushukuru.

Katika mchezo huo wa kwanza kwa kocha Mwambusi, alijikuta timu yake ikiwa nyuma kwa bao 1-0 kabla ya mapumziko kupitia bao maridadi la David Bryson kunako dakika ya 28 ya mchezo.

Kipindi cha pili Yanga walianza kwa kasi na kutupia bao la kuweka usawa dakika ya 46 kupitia kwa Yacouba Songne.

Sare hiyo inaifanya Yanga kufikisha jumla ya pointi 51 ikiwa nafasi ya kwanza huku KMC ikifikisha pointi 36 na ipo nafasi ya sita.

“Hatukupanga kupata pointi moja ila kwa kuwa siku zote nimekuwa nikisema tangu awali kuwa KMC huwa inakuwa bora ikikutana na Yanga na hata ukitazama nafasi yake bado inaonyesha ni timu yenye ushindani.

“Makosa ambayo yamejitokeza tunayafanyia kazi kwa ajili ya mechi zetu zijazo. Ninawapongeza wachezaji wangu kwa kuwa walipambana na bado hatujakata tamaa ya ubingwa,” .

Kwa sasa Yanga wanajiandaa na mchezo wa Aprili 17 dhidi ya Biashara United katika dimba la Mkapa saa 1 usiku.

Author: Asifiwe Mbembela