Kombora la Kompany laiweka Man City mkono mmoja kwenye taji

Manchester City watahifadhi taji lao la Ligi ya Premier kama watashinda mechi yao ya mwisho msimu huu baada ya kombora kali la nahodha Vincent Kompany kuizamisha Leicester iliyocheza kwa kujituma.

Huku zikiwa zimesalia dakika 20 mechi kumalizika, na matokeo yakiwa sifuri kwa sifuri na hofu ikiwa imetanda dimbani Etihad, mabngwa hao wa tetezi walihitaji muujiza katika mechi ambayo ni ushindi pekee ambao ungewarejesha kileleni mwa ligi.

Na wakaupata kutoka kwa mtu ambaye hakutarajiwa na wengi, kutoka kwa nahodha wao wa muda mrefu, ambaye aliandaa mpira na kuvurumisha shuti kali kutoka umbali wa hatua 25 hadi ndani ya wavu. Ushindi huo una maana City wanarejea tena kileleni mwa ligi mbele ya Liverpool na wana faida ya mwanya wa pointi moja wakati wakiingia katika mechi ya mwisho ya ligi siku ya Jumapili, wakati vijana wa Pep Guardiola watacheza ugenini dhidi ya Brighton nao wijana wa Jurgen Klopp watakuwa nyumbani dhidi ya Wolves.

Author: Bruce Amani