Kushika mpira kwenye 18 sio kosa tena, Sheria mpya ya kandanda Ulaya kutumika Euro 2020

Shirikisho la Kandanda barani Ulaya Uefa limesema kuanzia michuano ya Euro 2020 hakutakuwa na adhabu endapo mshambuliaji atashika, atagusa mpira wa bahati mbaya eneo la 18 wakati akiwa kwenye harakati za kufunga goli.

Mabadiliko hayo yalifanywa mwezi Machi na Bodi ya Sheria ya Kandanda Kimataifa na sasa yataanza matumizi kwenye michuano ijayo ya Euro 2020 inayoanza Juni 11, imewekwa wazi kuwa kwa sasa mashindano mbalimbali yanaweza kutumia kwa upendo wao.

Mwenyekiti wa marefarii ndani ya Uefa Roberto Rosetti amesema mabadiliko hayo ni katika kuboresha kandanda na radha yake.

Miongoni mwa matukio ya karibuni ambayo yalileta mgogoro ni pamoja na goli la Fulham dhidi ya Spurs lililokataliwa baada ya VAR kuonyesha mchezaji wa Fulham Mario Lemina alinawa mpira kwa bahati mbaya kabla kabumbu kumfikia mfungaji Josh Maja.

Hata hivyo, Rosetti amesema mpira unahusisha maamuzi yenye utata, hivyo kutahitaji umakini wa hali juu kabla ya kufikia maamuzi ya kukubali au kulikataa bao kwa kisingizo cha kunawa mpira kwa bahati mbaya.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares