Lampard akwama na Kepa, asema anahitaji kuungwa mkono katika makosa yake

153

Kocha mkuu wa kikosi cha Chelsea Frank Lampard amesema atajitahidi kurudisha makali ya mlinda mlango wake Kepa Arrizabalaga baada ya kufanya makosa mengine yaliyopelekea Chelsea kuambulia kipigo nyumbani Stamford Bridge dhidi ya Liverpool.

Chelsea ilikutana na kipigo cha goli 2-0 dhidi ya Liverpool katika mchezo wa Ligi Kuu nchini England raundi ya pili huku Kepa ambaye alikuwa analaumiwa kutokana na makosa, jana pia alifanya kosa lililopelekea goli la pili la Sadio Mane. Kipa huyo pia alifanya kosa katika mchezo wa ufunguzi wa pazia la EPL dhidi ya Brighton.

Makosa hayo yameifanya klabu ya Chelsea kuanza kutafuta mbadala wa Kepa Arrizabalaga ambaye amekuwa na makosa ya hapa na pale, jina la mlinda mlango wa Rennes Edouard Mendy linatajwa kuwa kipa wa The Blues msimu huu.

“Ni kweli ni makosa ya wazi ambayo yamekuwa yakitugharimu”, alisema Lampard akizungumzia mapungufu ya kipa huyo raia wa Hispania. “Tunatakiwa kuendelea kupambana, Kepa anatakiwa kuendelea kujifunza huku akiwa msaada wa karibu na sio kumshambulia hata kidogo”.

“Binafsi wachezaji wanahitaji msaada mkubwa ili kuanza kupata nguvu ya kufanya vizuri, nimekuwa karibu kwa kila mchezaji ili anieleze shida yake ili nijue nafanyaje”.

“Hakuna hata mmoja ambaye anajaribu kufanya makosa kwenye soka, hiyo ndio asili ya soka lenyewe. Kipa huyo wa kimataifa wa Hispania amekuwa kwenye ushindani wa namba ngazi ya taifa na mlinda mlango wa Manchester United David de Gea kwa muda sasa ingawa shida kubwa wote wapo katika kiwango duni kutokana na makosa binafsi ya kila mmoja.

Kepa, 25, anaendelea kushikilia rekodi ya kuwa mlinda mlango ghali zaidi ambapo alinunuliwa kwa pauni milioni 71 akitokea Athletic Bilbao miaka miwili iliyopita.

Muendelezo wa kiwango chake kibovu kumeiamusha Chelsea kumtafuta mlinda mlango wa Rennes Mendy, 28.

Author: Asifiwe Mbembela