Lampard arejea nyumbani darajani kama kocha mkuu

204

Chelsea imemtambulisha rasmi kiungo wa zamani wa timu hiyo Frank Lampard kuwa kocha wake mpya kwa kandarasi ya miaka mitatu kuanzi leo Julai 4.

Kutambulishwa kwa Lampard, 41, kunamaanisha anaachana na timu ya Derby County inayoshiriki Ligi daraja la pili England na kurejea darajani alipodumu kwa miaka 13 kama mchezaji.

Frank anachukua mikoba ya mtangulizi wake Maurizio Sarri, aliyeamua kuachana na klabu hiyo mwezi Juni kujiunga na Mabingwa wa Ligi ya Italia Juventus.

Akiwa Derby, Frank Lampard alikiongoza kikosi hicho mpaka fainali ya mchezo wa mtoano kufuzu kucheza ligi kuu msimu wa 2019/20 licha ya kupoteza dhidi ya Aston Villa katika hatua hiyo.

Lampard ni miongoni mwa wachezaji wenye heshima zaidi Chelsea akiwa amecheza mechi 648 na kushinda mataji makubwa 11 huku akishikilia rekodi ya kuwa mfungaji wa muda wote ndani ya “The Blues”.

Chelsea ipo katika kifungo cha kutosajili mchezaji hata mmoja kwa miaka miwili kutoka FIFA jambo ambalo Lampard lazima alitazame kwa makini.

“Nina furaha kubwa sana kurejea Chelsea kama kocha mkuu, kila mmoja anajua mapenzi yangu na hii klabu, hivi sasa naweka nguvu zangu kwenye maandalizi ya msimu ujao,” amesema Lampard baada ya kutambulishwa.

Lampard anakuwa kocha wa 10 kuajiliwa Chelsea chini ya mmiliki Roman Abramovich tangu achukue timu hiyo mwaka 2003.

Aliyekuwa kocha msaidizi Derby Country Jody Morris na kocha mazoezi Chris Jones wamekula shavu la kuungana na Lampard kujiunga na Chelsea ndani ya Stamford Bridge.

Lampard anaungana na Petr Cech ambaye aliteuliwa mwezi Juni kuwa Mshauri wa bechi la Ufundi Chelsea.

Author: Asifiwe Mbembela