Leipzig yainyoa Leverkusen na kuchukua nafasi ya tatu

Yussuf Poulsen alifunga bao moja katika kila kipindi na kuisaidia timu yake ya RB Leipzig kuirindima Bayer Leverkusen 3-0 Jumapili na kusonga katika nafasi ya tatu ya Bundesliga mbele ya mabingwa Bayern Munich.

Mwenzake Lukas Klostermann aliifungia Leipzig bao la pili  wakati wakipata ushindi wao wa pili mfululizo na kuendeleza matokeo yao ya kutopoteza mchuano wowote katika mechi kumi za ligi.

Leipzig sasa wana pointi 22 baada ya mechi 11 huku Borussia Moenchengladbach wakiwa katika nafasi ya pili na pointi 23 nyuma ya viongozi Borussia Dortmund ambao wana pointi 27, baada ya kutoka nyuma mara mbili na kuwabwaga Bayern 3-2 Jumamosi. Mabingwa Bayern wako katika nafasi za tano na pointi 20.

Kichapo cha pili mfululizo cha Leverkusen kinawaacha katika nafasi ya 13 na pointi 11 na kinamuweka kocha Heiko Herrlich katika shinikizo kubwa.

Kocha wa Schalke Domenico Tedesco pia aanakabiliwa na mbinyo baada ya timu yake kupoteza 3-0 dhidi ya Eintracht Frankfurt, ambao wamepanda hadi nafasi ya nne na pointi 20, mbele ya Bayern Munich na tofauti ya mabao.

Luka Jovic aliifungia Frankfurt mabao mawili na kuchukua usukani wa orodha ya wafungaji bora katika Bundesliga akiwa na mabao 9

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends