Leipzig yaizamisha Gladbach na kukamata nafasi ya tatu

49

RB Leipzig imefanikiwa kupanda kwenye msimamo Wa ligi kuu ya kandanda ya Bundesliga baada ya kupata ushindi dhidi ya Borrussia Monchengladbach. Leipzig ilipata magoli ya mapema na kuizamisha Borrussia Monchengladbach 2-0

Mshambuliaji wa Leipzig na timu ya taifa ya Ujerumani Timo Werner alifunga goli kwenye kipindi cha kwanza na kufanikiwa kuipa timu yake alama zote tatu. Matokeo hayo yameifanya RB Leipzig kukwea mpaka nafasi ya tatu ya msimamo kwa kukusanya alama 25 katika michezo 13 ambapo Monchengladbach inakamata nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya kukusanya alama 26 zote zikiwa zimecheza michezo Sawa na Leipzig.

Ligi hiyo itaendelea Disemba 8 ambapo Leipzig itasafiri kucheza dhidi za Freiburg huku Monchengladbach ikiwa nyumbani kumenyana vikali na wageni Stuttgart Jumapili ya wiki hii.

Eintracht Frankfurt 1-2 Wolfsburg

Wolfsburg ikiwa ugenini imeitwanga na  kupata ushindi wa jioni dhidi ya Eittracht Frankfurt wa goli 2-1 siku ya Jumapili.

Admir Mehmedi alifunga goli la kwanza baada kuipita ngome ya wageni, goli la pili likawekwa kimiani na Daniel Ginczek kunako dakika ya 68 na kuipa Wolfsburg matumaini ya kuendelea kufanya vizuri kwenye ligi ya Bundesliga.

Luka Jovic aliifungia Frankfurt goli la kufutia machozi dakika tatu kabla mchezo kumalizika halikusaidia lolote.

Matokeo hayo yameifanya Frankfurt kuangushwa mpaka nafasi ya tano katika msimamo wa Bundesliga kwa alama 23. Aidha Wolfsburg imepanda mpaka nafasi ya 8 ikiwa na alama 18 zote zikiwa zimecheza michezo sawa yaani 13.

Eintracht itakuwa ugenini kukipiga dhidi ya Hertha Berlin katika bilinge bilinge za kandanda nchini Ujerumani, ambapo Wolfsburg itaikaribisha Hoffenheim mchezo utapigwa siku ya Jumapili.

Author: Bruce Amani