Leipzig yawaomba radhi mashabiki wa Kijapan kwa ‘kosa’ la virusi vya corona

Klabu ya ligi kuu ya kandanda Ujerumani – RB Leipzig imeomba radhi kwa kikundi cha mashabiki wa Kijapan waliofurushwa uwanjani kutokana na hofu ya virusi vya corona. Wageni hao waliambiwa waondoke uwanjani katika mchuano wa Jumapili wa ligi kuu nyumbani dhidi ya Bayer Leverkusen. Leipzig imesema kuwa walinzi wake walihitajika kufanya ukaguzi mkali dhidi ya vikundi au watu kutoka maeneo yanayozingatiwa kuwa kwenye kitisho kikubwa cha virusi hivyo.

Klabu hiyo imekiri kufanya kosa na kuwa italirekebisha. Leipzig inapanga kuwaalika wageni hao wa Kijapan kwa mtanange wao ujao katika uwanja wa nyumbani. Klabu hiyo haikutoa maelezo zaidi ya tukio hilo. Hata hivyo shirika la habari la Ujerumani DPA limesema kikundi cha wageni 20 wa Kijapan waliambiwa waondoke uwanjani karibu dakika 10 kabla ya mchezo kuanza. Mechi hiyo ilikamilika kwa sare ya 1 – 1 na kuwaacha nambari mbili Leipzig wakiwa na pengo la pointi tatu nyuma ya vinara Bayern Munich.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends