Leverkusen na Bayern, nani atatwaa Kombe la Shirikisho Ujerumani?

177

Mabingwa mara nane mfululizo wa ligi ya soka Ujerumani Bundesliga, Bayern Munich Jumamosi (04.07.2020) watashuka dimbani kumenyana na Bayer Leverkusen katika fainali ya kombe la shirikisho, DFB Pokal.

Bayern ambao walifanikiwa kulitwaa taji la Bundesliga katika msimu uliomalizika, msimu uliobadilishwa na mlipuko wa virusi vya Corona, kwa sasa wanatamani tena kuongeza taji lengine.

Kinyume chake timu ya Leverkusen haijaonja mafanikio tangu mwaka 1993 licha ya kunyemelea kwa karibu kulitwaa taji la Bundesliga takriban mara nane, kombe la DFB Pokal pamoja na ligi ya mabingwa barani Ulaya.

“Tutaendelea kuwa na njaa,” alisema mchezaji wa Bayern, Joshua Kimmich, baada ya kufanikiwa kulitwaa taji la Bundesliga. Bayern walipoteza fainali ya kombe la shirikisho 2018 dhidi ya Eintracht Frankfurt.

Matumaini ya kurudia tena kushinda mataji matatu kama 2013 bado yapo huku ligi ya mabingwa wa Ulaya ikitarajiwa kurejea tena dimbani mwezi Agosti mwaka huu. Bayern wanakaribia kufuzu katika robo fainali, baada ya kushinda mechi yao ya ugenini dhidi ya chelsea kwa idadi ya kutosha ya magoli.

Author: Bruce Amani