Ligi ya Hispania kurudi Juni 12 amesema Rais wa La Liga Javier Tebas

Rais wa La Liga Javier Tebas amesema ana matumaini ya ligi kuu nchini humo kurejea mwezi Juni 12 ambapo anaamini pia kufikia tarehe hiyo hakutakuwa na maambukizi ya virusi vya Corona kwa wachezaji wa vilabu vyote tofauti na ilivyo hivi sasa.

Viongozi wa ligi siku ya Jumapili walitoa taarifa kuwa wachezaji watatu walipimwa na kukutwa wameathirika na Covid-19 katika ligi mbili (daraja la kwanza na pili). Hii inakuja kipindi ambacho wachezaji wa La Liga wameshaanza kurudi katika viwanja vya mazoezi.

“Nitapendelea zaidi kuanza michezo Juni 12,” alisema Tebas.

“Lakini tunatakiwa kuwa makini sana. Ligi inatakiwa ilijee lakini itategemeana na athari za ugonjwa huo katika kipindi hicho kwani hatufanyi hili pekee yetu bali kama jamii ya Kihispania”.

Tebas aliongeza kwa kusema ligi daraja la pili litaanza sawa na ligi kuu kwani mashindano yote nchini humo inatakiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi Julai yaani 31 Julai ili kutoa nafasi ya mashindano ya Ulaya kumalizika.

Taifa la Hispania limekuwa miongoni mwa nchi ambazo zimeathirika vibaya na janga la Corona kwani mpaka leo Mei 11 vifo 26,621 na waathirika 264,663 wamesharipotiwa.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends